Tatizo la uhaba wa maji katika kaunti ya Kilifi limeendelea kugonga vichwa vya habari, bila ya kupata suluhu la tatizo hilo la mda mrefu.
Hii ni baada ya wakaazi kulalamikia kukosa maji kwa mda mrefu na kuchangia maandamano, ya vipi punde ikiwa ni wakaazi wa Bamba eneo bunge la Ganze, ambao katika maandamano yao walifunga ofisi ya Mwakilishi wadi ya Bamba Mohammed Mwambire.
Purukushani, mivutano na hatimaye vurugu, zilishuhudiwa nje ya ofisi ya Mwakilishi wadi hiyo na kusababisha wengine kupata majeruhisa.
Wakaazi hao walisisitiza kwamba ni lazima serikali ya kaunti ya Kilifi kupitia Mwakilishi wadi wao kuhakikisha eneo hilo la Bamba linapata huduma bora za maji safi kwa matumizi kwani wamehangaika kwa mda mrefu ama wataendelea na maandamano.
Mapema siku ya Alhamis Oktoba 23, Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alililaumu shirika la usambazaji maji kanda ya Pwani kutokana na uhaba wa maji unaoshuhudiwa pamoja na kukarabati visima vya maji vilivyoharibika.
Akijibu lalama hizo zilizoibuliwa na serikali ya kaunti ya Kilifi kuhusu changamoto za maji, Mwenyekiti wa Shirika la huduma za usambazaji maji kanda ya Pwani, Dkt Daniel Mwaringa alikosoa kauli zilizotolewa na viongozi wa serikali hiyo, akisema Shirika hilo kukatiza huduma za maji kaunti ya Kilifi ni kutokana na kaunti hiyo kushindwa kulipa malimbikizi ya madeni kwa wakati.
