Brendan Rodgers amejiuzulu kama kocha wa Celtic na Martin O’Neill kuteuliwa

Brendan Rodgers amejiuzulu kama kocha wa Celtic na Martin O’Neill kuteuliwa

Mkufunzi wa kilabu ya Celtic Brendan Rodgers amejiuzulu kama kocha wa kilabu hiyo  hatua iliyojiri baada ya tuhuma kutoka kwa mwenyehisa mkuu Dermot Desmond aliyemshutumu kwa “tabia ya kugawanya, kupotosha, na kujitakia makuu”  na atachukuliwa nafasi kwa muda na aliyekuwa kocha wa zamani, Martin O’Neill.

Mabingwa wa Scottish Premiership wameporomoka hadi pointi nane nyuma ya vinara wa ligi Hearts, baada ya kupoteza kwa urahisi katika uwanja wa Tynecastle Jumapili, wakiwa na kampeni dhaifu barani Ulaya na dirisha la usajili lililojaa sintofahamu.

Ingawa kulikuwa na hali ya kutoridhika katika Celtic Park, taarifa iliyotolewa na klabu saa 3:44 usiku GMT iliwashangaza wengi.

Taarifa hiyo yenye maneno 134 ilitangaza kwamba Rodgers amejiuzulu, ikimshukuru kwa mchango wake katika vipindi vyake viwili kama kocha wa timu hiyo, na kueleza kuwa mchakato wa kumpata mbadala wake umeanza.

Katika mabadiliko ya kushangaza, taarifa hiyo pia ilibainisha kuwa Martin O’Neill  mwenye umri wa miaka 73 na miaka 20 tangu kipindi chake cha kwanza kumalizika atachukua majukumu ya muda, akisaidiwa na Shaun Maloney, mchezaji wa zamani wa Celtic ambaye alifutwa kazi kama kocha wa Wigan Athletic mwezi Machi.