Rais William Ruto amepongeza klabu ya Nairobi United Football Club kwa kuandika historia kwa kufuzu kwa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF (CAF Confederation Cup) kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Rais Ruto alieleza mafanikio hayo kama “wakati wa fahari kubwa ya kitaifa” na ushahidi wa ukuaji wa hadhi ya Kenya katika soka la Afrika.
“Hii ni hatua ya kipekee, iliyojengwa kwa ujasiri, nidhamu na uvumilivu usioyumba. Ushindi huu umechochea ari ya taifa letu na kuthibitisha nafasi halali ya Kenya katika ramani ya soka la Afrika,” alisema Rais Ruto katika taarifa yake.
Kevin Oduor alijitokeza kuwa shujaa wa mechi hiyo baada ya Nairobi United kuishinda Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia kwa mikwaju ya penalti 7-6, na hivyo kufuzu kwa hatua ya makundi ya michuano hiyo ya kifahari Jumapili usiku.
Kipa huyo aliokoa penalti mbili muhimu wakati Naibois (jina la utani la timu hiyo) waliandika historia kwa kufuzu kwa mara ya kwanza katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Wawakilishi hao wapya wa Kenya barani Afrika walikuwa na faida ya mabao 2-0 kutoka mechi ya kwanza jijini Nairobi, lakini wenyeji walirejesha matokeo kwa ushindi wa 2-0 katika muda wa kawaida, na hivyo kufanya jumla ya 2-2, kabla ya pambano kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Kwa kufuzu kwa hatua ya makundi, Nairobi United watavuna takriban Shilingi milioni 51 kama zawadi kutoka CAF.
