Watu 12 wahofiwa kufariki baada ya ndege kuanguka Kwale

Watu 12 wahofiwa kufariki baada ya ndege kuanguka Kwale

Watu 12 wanahofiwa kufariki baada ya ndege ndogo ya utalii kuanguka katika eneo la Tsimba gatuzi dogo la Matuga kaunti ya Kwale.

Ndege hiyo ilikuwa imetokea eneo la Diani kuelekea Kichwa Tembo kwa shughuli za kiutalii katika eneo la Masai Mara kabla ya kuanguka na kuchomeka.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya usafiri wa anga nchini KCAA, Emile Arao, alisema ndege hiyo ndogo yenye nambari ya usajili 5Y-CCA ilikuwa na abiria 12 wenye asili ya Ugerumani ambao walikuwa wameabiri ndege hiyo.

Arao alisema tayari maafisa wa usafari wa angani wameanzisha uchunguzi ili kubaini kiini cha ajali hiyo kwani hata mabaki ya ndege hiyo yalichomeka.

 

Taarifa ya Mamlaka ya usafiri wa anga nchini KCAA kuhusu kuanguka kwa ndege ya 5Y-CCA

Ajali hiyo ya ndege imetokea miezi kadhaa baada ya ndege ndogo ya Wanajeshi kuanguka katika kaunti hiyo ya Kwale kutokana na changamoto za kimitambo.

Hii sio mara ya kwanza mikasa ya ndege kuanguka kushuhudiwa katika ukanda wa Pwani ambapo ndege yengine ndogo ilikuwa katika mafunzo ya marubani ilikumbwa na hitilafu za kimitambo na kuanguka katika eneo la Kwa Chocha mjini Malindi.

Ajali hiyo ya Malindi ilisababisha vifo vya watu wawili ingawa changamoto kubwa ni kwamba hakujakuwa na taarifa zozote kuhusu ripoti ya kilichosababisha ajali hiyo na hata fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.