Kamati kuu ya Chama cha ODM imemuidhinisha Seneta Dkt Oburu Oginga kuwa Kaimu Kinara wa Chama hicho.
Katibu mkuu wa ODM Edwin Sifuna, alisoma taarifa ya pamoja na Kamati hiyo ambayo imewataka viongozi wengine wa chama hicho kumpa Oburu ushirikiano mwema wakati huu wa kipindi kigumu.
Katika taaifa hiyo, Chama cha ODM kilisema kitaendelea kupigania haki za wakenya, usawa na amani, jinsi Hayati Raila Odinga alivyokuwa akifanya humu nchini na hata mataifa mengine.
Wakati huo huo Chama hicho kimeshikilia msomamo wake wa kusalia katika serikali jumuishi yani broadbased Government hadi mwaka 2027, kwa kuendeleza mshikamano wa chama na wafuasi wa ODM ili kudhibiti migawanyiko katika chama hicho.
Chama hicho kupitia Katibu wake mkuu, kilisema kitaandaa ibada maalum kwa ajili ya Hayati Raila Odinga katika maeneo mbalimbali nchini, kaunti ya Kilifi, ibada hiyo itaandaliwa katika eneo la Magarini, Novemba tarehe 2 na tarehe 3.
Chama hicho hata hivyo kilisema kitaendelea na mikakati yake ya kuwasajili wanachama zaidi katika chama hicho pamoja na kufungua ofisi katika maeneo ili kufanikisha mipango na mikakati ya Hayati Raila.
