Mahakama ya Shanzu imeagiza washukiwa sita wa ulanguzi wa dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine zenye thamani ya shilingi bilioni 8.2 kusalia korokoroni kwa siku 30 ili kufanikisha uchunguzi.
Hakimu mkuu wa Mahakama ya Shanzu Anthony Mwicigi aliagiza washukiwa hao kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Bandari na kupewa huduma muhimu za matibabu.
Mwicigi ameagiza pia 6 hao kurejeshwa Mahakamani mnamo tarehe 14 mwezi Novemba ambapo ripoti ya uchunguzi wa kiafya itatolewa na kisha kesi hiyo kusikizwa mnamo tarehe 27 mwezi huo wa Novemba.
Afisa mkuu wa upelelezi katika kesi hiyo Shadrack Kemei aliambia Mahakama kwamba kati ya washukiwa hao 6 waliokamatwa, wanne pekee ndio raia wa Iran huku wawili wakiwa bado hawajatambuliwa uraia wao.
Kemei alisema shehena ya dawa za kulevya pamoja na vifaa vya mawasiliano vilivyokamatwa vitahitaji kufanyiwa uchunguzi kwenye maabara ya Serikali ili kubaini uhalisia wa dawa hizo.
“Kati ya washukiwa hawa 6 waliokamatwa, wanne pekee ndio raia wa Iran na wawili bado hawajatambuliwa uraia wao na bado tunafanya uchunguzi kuhusu dawa hizo za kulevya kwani shehena iliyokuwa na dawa hizo ni kubwa sana lakini bado tunafuatilia kubaini mmiliki halisi wa shehena hiyo”, alisema Kemei.
Wakati huo huo Kemei aliomba Mahakama kutowapa dhamana washukiwa hao, akisema ni tishio kwa usafiri kwani huenda wakahitilafiana na uchunguzi, huku akidokeza kuwa huenda 6 hao wanajumuisha mtandao mkubwa wa walanguzi dawa za kulevya.
Kauli yake ilisisitizwa zaidi ya kiongozi wa mashtaka Anthony Musyoka ambaye ameiomba Mahakama kuendelea kuwazuia sita hao kwa siku zaidi ili kukamilisha uchunguzi na kubaini iwapo dawa hizo zilikuwa zinaelekezwa kwa nani.
Taarifa ya Joseph Jira
