Chama cha UDA kimetangaza kumuunga mkono aliyekuwa Spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Jimmy Kahindi, kugombea wadhfa wa ugavana wa kaunti ya Kilifi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Katibu mkuu wa Chama cha UDA Hassan Omar Sarai alisema Chama hicho kimechukua uamuzi huo baada ya Mwenyekiti wa bodi ya Halmashauri ya barabara nchini Aisha Jumwa kukihama chama cha UDA.
Akizungumza katika kaunti ya Kericho wakati wa kikao cha kuhamasisha umma kuhusu uchaguzi wa viongozi wa mashinani, Sarai alisema kila mmoja ana haki ya kuwania wadhfa wowote wa kisiasa kwani demokrasia ya Kenya inaruhusu.
Sarai aliweka wazi kwamba chama cha UDA kitasimamisha wagombea wa nyadhfa mbalimbali kote nchini katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027, akisema chama hicho kimejipanga vyema katika uchaguzi huo.
Hatua hiyo imejiri baada ya Aisha Jumwa wiki iliyopita kutangaza wazi kwamba alikihama chama cha UDA na kujiunga na Chama cha PAA kinachoongozwa na Spika wa bunge la Seneti Amason Jeffah Kingi.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
