Mshukiwa wa ulaghai mtandaoni akamatwa Mombasa

Mshukiwa wa ulaghai mtandaoni akamatwa Mombasa

Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI eneo la Nyali kaunti ya Mombasa wamemkamata mshukiwa wa utapeli anayedaiwa kuwalaghai wageni wanaotafta nyumba za kukodisha kupitia mtandaoni maarifu Air BnB jijini Mombasa.

Mshukiwa huyo anayefahamika kama Brian Masika, inadaiwa amekuwa akiwavutia wateja wake kupitia picha nzuri za nyumba aliyoiita “Brima Mangu Apartment 2B,” na kuwatoza fedha kisha kutoweka.

Inasemekana mnamo Disemba 1,2025, mkazi mmoja wa Nairobi alituma shilingi elfu ishirini na nne baada ya kuamini tangazo hilo la kupendeza lakini alipowasili Mombasa tarehe 4 Disemba, juhudi zote za kumpata Masika zikagonga mwamba, na familia yake kusalia bila makazi.

Baada ya kuripoti tukio hilo, DCI walianzisha msako mkali na kwa msaada wa taarifa za kiteknolojia, walifanikiwa kumkamata mshukiwa ambaye sasa anazuiliwa na maafisa wa polisi kabla ya kufikishwa kortini.

DCI iliwarai wananchi na wageni kuwa waangalifu wanapotafuta nyumba za kukodi mtandaoni, kwani ulaghai umeongezeka kipindi hiki cha shamra shamra za sikukuu ya Krisimasi na mwaka mpya.

Taarifa ya Mwanahabari wetu.