Mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya bandari nchini, nahodha William Ruto, ameibua matumaini mapya kuhusu uboreshaji wa Bandari ya Mombasa baada ya kutangaza hatua mbalimbali za kisasa zinazolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za bandari.
Akizungumza kwenye kikao na viongozi wa chama cha mawakala wa forodha nchini (KIFWA), nahodha Ruto alisema KPA imeanza kutekeleza miradi muhimu kama kudhibiti kina cha bahari kwa ajili ya kupokea meli kubwa, ujenzi wa Gati ya kwanza katika eneo la Dongo Kundu, pamoja na uendelezaji wa Gati 19B ili kupanua uwezo wa bandari ya Mombasa kushughulikia mizigo zaidi.
Alieleza kuwa KPA pia imewekeza kwenye mitambo ya kisasa yenye ufanisi wa nishati, ikiwemo kreni za ‘rubber-tyred gantry’, hatua ambayo itapunguza muda wa meli kukaa bandarini na kuongeza kasi ya kazi.
Katika hatua nyingine, Ruto alisema utekelezaji wa mifumo ya kiotomatiki utaongeza kasi ya huduma hususan kwenye lango la bandari, akibainisha kuwa mageuzi ya kidijitali ndiyo dira ya kufanikisha shughuli za bandari kwa viwango vya kimataifa.
Pia alisisitiza umuhimu wa bandari ya Lamu, akisema kituo hicho kinazidi kuimarika kama nguzo muhimu ya mradi wa LAPSSET, huku akialika viongozi wa KIFWA kufanya ziara ya kujifunza kwenye bandari hiyo.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa KIFWA kanda ya Pwani, Rajab Hamisi, aliwapongeza wanachama kwa kazi yao thabiti, na kuishukuru KPA kwa kuendeleza ushirikiano unaolenga kuongeza ushindani na ufanisi katika sekta ya usafirishaji.
Taarifa Mwanahabari wetu.
