Wakili na mwanasiasa, George Kithi, hatimaye ameweka mambo wazi kuhusu madai yaliyokuwa yakisambaa kwamba alikuwa nyuma ya mpango wa kumleta msanii maarufu wa Tanzania, Zuchu, kutumbuiza Kaunti ya Kilifi.
Akizungumza wakati wa hafla ya Influencersâ Gala iliyofanyika katika hoteli moja eneo la Kilifi, Kithi alisema alishtushwa pia kujikuta akihusishwa na simulizi hiyo kama mratibu au promota wa tukio hilo, akieleza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote na yamebuniwa.
Alibainisha kuwa alichukua hatua zaidi kwa kuwasiliana na uongozi wa Zuchu ili kufahamu ni nani hasa anayedaiwa kuwa anampanga msanii huyo kuja kutumbuiza katika kaunti yake ya nyumbani.
Akihutubia waandaaji wa maudhui (influencers), Kithi aliwahimiza kutumia majukwaa yao kuhamasisha usajili wa wapiga kura, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi cha Gen Z.
âIkiwa taarifa isiyo na msingi inaweza kusambaa kwa kiwango hicho, basi inaonyesha kuwa mnaaminika sana na wafuasi wenu. Huo ni ushahidi wa nguvu kubwa mliyonayo kama influencers. Tumieni majukwaa haya kuhamasisha Gen Z na wananchi wengine kujisajili kama wapiga kura. Wanawaamini na kufuata mnachosema karibu kila wakati. Hawawaamini wanasiasa, lakini wanawaamini ninyi,â alisema George Kithi.
Kwa muktadha, kumekuwa na gumzo kubwa mtandaoni likidai kuwa Zuchu angepiga show Kaunti ya Kilifi wakati wa mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya. Hata hivyo, madai hayo yaliibua hisia mseto, huku baadhi ya wasanii wakipinga wazo hilo wakisema kuwa ingawa Zuchu hupata mamilioni akitumbuiza nchini Kenya, wasanii wengi wa ndani bado wanaendelea kuteseka kifedha.
Hafla ya Kilifi Content Creators Gala, iliyoandaliwa na Coco FM kwa ushirikiano na George Kithi Foundation na Ndani Media, inalenga kuinua tasnia ya uundaji maudhui, kuwawezesha influencers kwa ujuzi wa kuchuma mapato kupitia kazi zao, na kuhimiza ushirikiano kwa maendeleo chanya na endelevu katika anga ya kidijitali.
