Gavana wa kaunti ya Kilifi Gedion Mungâaro ametoa hutuba kuhusu mustakabili wa kaunti akiangazia masuala mbalimbali, huku suala la afya likipewa kipau mbele.
Hutuba hiyo iliyodumu kwa zaidi ya saa mbili katika bunge la kaunti ya Kilifi mjini Malindi, iliweka wazi jinsi kaunti ilivyopunguza deni iliyokuwa ikidaiwa na Mamlaka ya usambazaji dawa nchini KEMSA.
Gavana Mungâaro alisema serikali yake imehakikisha dawa hospitalini zinapatikana, vituo vya afya zaidi vinaidhinishwa sawa na kuhakikisha huduma bora za afya zinatekelezwa.
Kuhusu suala la maji, ambalo liligonga vichwa vya habari, gavana Mungâaro alisema bado kuna changamoto, akidokeza kuwa kaunti ya Kilifi kufikia sasa inapokea asilimia 60 ya maji kutoka mradi wa maji wa Baricho, akiitaka serikali kuu kuhakikisha awamu ya pili ya mradi wa Baricho unawanufaisha wakaazi wa Kilifi.
Aidha alidokeza kuwa serikali ya kaunti imelipa kipaumbele suala la kilimo ili kuhakikisha sekta hiyo inafanya vyema zaidi, sawa na kuboresha sekta ya elimu.
Taarifa ya Joseph Jira
