Kampeni za uchaguzi mdogo zatamatika rasmi

Kampeni za uchaguzi mdogo zatamatika rasmi

Kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge, useneta na uwakilishi wadi katika maeneo mbalimbali, zinatarajiwa kutamatika rasmi siku ya Jumatatu Novemba 24 mwaka huu wa 2025, saa kumi na mbili jioni.

Hii ni baada ya Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kupitia Mwenyekiti wake Erastus Ethekon kutangaza kipindi cha kampeni kuanza Oktoba 8 hadi Novemba 24 na kwamba zinafaa kufanyika kwa amani.

Katika kampeni hizo za lala salama kabla ya dirisha la kampeni kufungwa rasmi na Tume ya IEBC, viongozi mbalimbali ikiwemo wale wa Serikali na upinzani walionekana kuonyeshana ubabe wa kisiasa katika kampeni hizo.

Wazee wa Kaya za mijikenda katika eneo la Pwani, Wakiongozwa na Mratibu wa Wazee hao Tsuma Nzai Kombe, wameitaka Tume ya IEBC kuhakikishia chaguzi hizo zinakuwa huru na haki ili kudumisha amani nchini.

“Sisi kama wazee wa Kaya tunataka uchaguzi uwe huru na haki na maafisa wa IEBC wahakikisha wanaandaa uchaguzi wa amani ili kila mmoja awe na haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka. Hapa Magarini tunataka amani na sio vurugu kwa sababu watu wenyewe wa Magarini wanapenda amani”, walisema wazee hao.

Kamishna wa IEBC Alutalala Mukhwana amewahakikishia wakenya uchaguzi huru na haki huku akionya kuchukuliwa hatua za kisheria kwa viongozi wanaolenga kuzuru vurugu wakati wa uchaguzi.

“Sisi kama IEBC tumejipanga na tunawaambia watu wa Magarini na kwengine ambako uchaguzi utafanyika kwamba utakuwa huru na haki na maafisa wote wamepewa mafunzo kuhakikisha unatekeleza majukumu yao vyema”, alisema Alutalala.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi