Beacco: Serikali itahakikisha wafungwa wanawezeshwa ili kusaidia jamii zao

Beacco: Serikali itahakikisha wafungwa wanawezeshwa ili kusaidia jamii zao

Katibu katika Idara ya huduma za magereza nchini Dkt. Salome Beacco amesema serikali itahakikisha wafungwa wanapata mazingira bora ya afya, elimu na jamii ili kuwawezesha kurejea katika jamii wakiwa watu waliobadilika.

Dkt. Beacco alisema serikali inaendeleza mpango wa kuboresha magereza nchini, ikiwemo kutoa vitanda vipya, mavazi, huduma za maji safi na mafunzo ya stadi za maisha kwa wafungwa pamoja na kushughulikia maslahi ya maafisa wa magereza.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maktaba iliyoboreshwa katika gereza la Jela baridi eneo la Mvita kaunti ya Mombasa, Dkt. Beacco alisema mradi huo ulifadhiliwa na jamii ya Dawoodi Bohras, utachangia kuwapa wafungwa matumaini na dira mpya maishani.

“Tuko na mipango bora kama serikali kuhakikisha wafungwa wanawezeshwa na kuwa katika mazingira bora ya afya, elimu na jamii ili kuwawezeshwa kurejea katika jamii wakiwa watu waliobadilika”, alisema Beacco.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika linaloshughulikia waraibu na wagonjwa wa afya ya akili, Amina Abdallah alieleza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi katika kuendeleza miradi ya maendeleo kwenye magereza.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi