Zaidi ya Waogeleaji 300 Kushiriki Mashindano ya Kiambu Aquatics Masters Mwaka 2025

Zaidi ya Waogeleaji 300 Kushiriki Mashindano ya Kiambu Aquatics Masters Mwaka 2025

Mashindano ya Kiambu Aquatics Annual Masters Swimming Championships yanatarajiwa kuibua msisimko mkubwa Jumamosi, Novemba 29, 2025.

Wapenzi wa mchezo huo watakuwa wakielekeza macho yao yote katika Shule ya Potterhouse, Runda, ambako toleo la mwaka huu tayari limevunja rekodi kwa kuvutia idadi kubwa zaidi ya washiriki katika historia yake — ishara kwamba Masters Swimming nchini Kenya sasa imepata nafasi yake rasmi katika jukwaa kuu la michezo.

Mashindano ya mwaka huu yamepita matarajio yote, yakiwa na zaidi ya waogeleaji 300 na timu 45 zilizojitayarisha kushiriki. Tukio hilo limekuwa alama ya mwamko mkubwa wa uogeleaji wa Masters nchini Kenya.

Gedion Kioko, gavana wa Kiambu Aquatics na mwogeleaji wa kimataifa mashuhuri wa Masters, amesema mwitikio mkubwa wa mwaka huu unaonyesha ukuaji wa mchezo huo.

“Mwitikio huu unaonyesha kuwa uogeleaji wa Masters si suala la umri, bali ni kuhusu shauku na azimio la kuendelea kushindana,” alisema Kioko.

Vilabu kutoka kote nchini na hata nje ya Kenya vimekusanyika Runda kwa hafla hii ambayo inaahidi kuwa wikendi ya kasi, ustahimilivu, na ushindani mkali.

Miongoni mwa vilabu vitakavyoshiriki ni The Harpoons, Crawfordians, Genesis Swim Club, Tipwa Tipwa, United Swimming Club, Water Warriors, Parklands Sports Club, NextGen, Peponi School, Nakuru Athletics Swim Club, Arukah Health, SDPK, Safaricom PLC, Comprehensive Swim Fitness, Olive Fin, Hospital Hill Alumni, USIU-Africa, Potterhouse Team, Kenya Airways, na Team Tanzania.

Ratiba ya uogeleaji nchini bado ni imejaa matukio. Kuanzia Novemba 1–2, 2025, mashindano ya Inter-County Invitational Swimming Championship yatafanyika katika Mpesa Foundation Academy, Thika, yakivutia waogeleaji bora kutoka kote nchini.

Mashindano hayo yataonesha ubora wa michezo na kuweka msingi wa msimu wa Kiambu Aquatics Swimming League 2025–2026.

Wakati huo huo, bendera ya Kenya tayari inapepea juu nje ya nchi. Waogeleaji tisa wa Masters kutoka Kenya wakiongozwa na Kocha Jacqueline Macharia wa Kiambu Aquatics wanaiwakilisha nchi katika Mashindano ya Kwanza ya Zimbabwe Masters Swimming Championship huko Harare.

Ushiriki wao kwa gharama binafsi unaonyesha uvumilivu, kujitolea, na mapenzi ya kweli kwa mchezo, ukithibitisha kwamba shauku si ufadhili  ndiyo injini ya uhai wa uogeleaji wa Masters.