Timu ya Harambee Starlets imefuzu rasmi kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuishinda Gambia 1-0

Timu ya Harambee Starlets imefuzu rasmi kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuishinda Gambia 1-0

Timu ya Harambee Starlets imefuzu rasmi kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuishinda Gambia 1-0 katika mechi ya marudiano ya raundi ya tatu iliyochezwa Jumanne jioni kwenye Uwanja wa Stade Lat Dior mjini Thies, Senegal. Ushindi huo uliwapa jumla ya ushindi wa 4-1 kwa jumla ya mikondo miwili, baada ya kupata ushindi wa 3-1 katika mchezo wa kwanza jijini Nairobi Ijumaa iliyopita.

Baada ya kipindi cha kwanza kilichokuwa na mashambulizi ya pande zote mbili, Mwanahalima Adam Jereko alifunga bao la ushindi katika dakika ya 59 lililotosha kutuma kikosi cha Beldine Odemba kwenye michuano ya bara la Afrika itakayofanyika kuanzia Machi 17 hadi Aprili 3 mwaka 2026 nchini Morocco — hii ikiwa ni mara ya pili kwa Kenya kushiriki, baada ya mara ya kwanza mwaka 2016 mjini Yaoundé, Cameroon.

Mbele ya lango, mshambulizi Shirleen Opisa alipata nafasi nzuri ya kuifungia Kenya katika dakika ya 24, lakini shuti lake lilizuiliwa vyema na kipa wa Gambia, Aminata Gaye. Kwa upande mwingine, mshambulizi hatari wa Gambia anayekipiga katika Ligi Kuu ya Wanawake Hispania na klabu ya Sevilla, Fatou Kanteh, alikaribia kusawazisha katika dakika ya 74, lakini kipa Lilian Awuor alifanya kazi nzuri kuokoa.

Mbali na kufuzu kwa mara ya pili kwenye WAFCON, wachezaji wa Starlets watapokea KSh 1 milioni kila mmoja kutoka kwa Rais William Ruto, aliyekuwa ameahidi zawadi hiyo iwapo wangepata ushindi na kufuzu.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Nairobi, mabao kutoka kwa Mwanahalima Adam, Fasila Adhiambo, na Shirleen Opisa yaliwapa Kenya uongozi mzuri na kujiamini kuhitimisha kazi katika marudiano.

Kenya ilishiriki kwa mara ya kwanza katika WAFCON 2016 nchini Cameroon, lakini haikupata ushindi wowote hatua ya makundi. Starlets waliwekwa kundi moja na Nigeria (waliotwaa taji), Mali, na Ghana. Walianza kampeni kwa kupoteza 3-1 dhidi ya Ghana, wakapoteza tena 3-1 dhidi ya Mali, na kufungwa 4-0 na Nigeria katika mechi yao ya mwisho ya makundi.

Safari yao kuelekea Morocco 2026 imekuwa ya uvumilivu na imani. Kabla ya kuivurumisha Gambia, Starlets waliitoa Tunisia katika raundi iliyotangulia kwa ushindi wa 1-0 ugenini baada ya sare jijini Nairobi ushindi uliowezeshwa na uchezaji bora wa kipa Lilian Awuor, aliyepangua penalti mbili muhimu na kudumisha ndoto ya Kenya kufuzu tena kwa fainali hizo.