Maelfu ya wakaazi wajitokeza kwenye matibabu ya bila malipo chuo kikuu cha pwani

Maelfu ya wakaazi wajitokeza kwenye matibabu ya bila malipo chuo kikuu cha pwani

Wiki ya matibabu ya bila malipo ya mwaka 2025 inakamilika jumapili  ya tarehe 2, Novemba 2025, katika chuo kikuu cha Pwani kaunti ya kilifi, huku ikivutia maelfu ya wakaazi waliowasili kutafuta huduma za matibabu.

Wakaazi waliofika katika kambi hiyo ya matibabu walisema zoezi hilo linawapa fursa adimu ya kupata suluhu kwa matatizo yao ya kiafya, ambapo dawa za matibabu imekuwa changamoto kwa kuzifikia.

Wakaazi mmoja baada ya mwengine walieleza hisia zao kuhusiana na zoezi hili lililoasisiwa na wakfu wa wakili George Kithi, Chuo kikuu cha Pwani, COCOFM na wadau mbalimbali.

Akizungumza katika chuo kikuu cha pwani kunakoendelea zoezi hilo, mkurugenzi wa George Kithi Foundation, wakili George Kithi alisema wakaazi wa kaunti ya Kilifi wanauhitaji mkubwa wa huduma bora za afya.

Kithi alidokeza kuwa zoezi hilo litakuwa likifanywa mara kwa mara ili kuhakikisha wakaazi wa Kilifi na Pwani kwa jumla wanafikia huduma bora za afya, ili jamii iweze kuwa yenye afya inayostahili.

Wakili George Kithi akitembelea baadhi ya wagonjwa katika chuo kikuu cha pwani Kilifi.

Kwa upande wake mhadhiri wa chuo kikuu cha pwani profesa Halim Shauri, alipongeza uanzilishi wa mpango huo akidokeza kuwa chuo kikuu cha pwani kina mikakati ya kujenga hospitali kuu ambayo mbali na kutoa mafunzo ya kitaalamu, pia itasaidia kutoa huduma za afya kwa wakaazi wa pwani.

Baadhi ya wagonjwa waliofika katika chuo kikuu cha Pwani mjini Kilifi kupokea matibabu ya bila malipo.

Naye naibu msimamizi wa mpango wa kambi ya wiki ya matibabu ya bila malipo katika wakfu wa George Kithi daktari Julius Nyamawi, amesema zoezi hili limefaidi wakaazi wengi ambao wamekuwa na changamoto ya kupata matibabu.

Taarifa ya Joseph Jira