Klabu ya Soka ya Ulinzi Stars, inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Jumatatu ilimfuta kazi kocha mkuu Dunstan Nyaudo kufuatia msururu wa matokeo mabaya katika ligi hiyo ya juu.
Mabingwa wa zamani wa KPL walitangaza katika taarifa kwamba kocha huyo ameachishwa majukumu yake “mara moja.”
“Uongozi unathamini kujitolea, taaluma na huduma ya Kocha Nyaudo kwa timu, ndani na nje ya uwanja, wakati wote akiwa madarakani.
Tunamshukuru kwa dhati kwa mchango wake kwa familia ya Ulinzi Stars na tunamtakia mafanikio mema katika safari yake ijayo,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Timu hiyo ya wanajeshi imekuwa na msimu mgumu, ikishinda mechi moja pekee kati ya tano walizocheza hadi sasa. Wako nafasi ya 13 kati ya timu 18 kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi 5 kutokana na michezo hiyo mitano.
Uamuzi huo unamaliza kipindi cha tatu cha Nyaudo kama kocha mkuu wa timu hiyo ya kijeshi, ukifunga sura nyingine katika uhusiano wake wa muda mrefu na Ulinzi Stars.
Akiwa mchezaji kati ya mwaka 1993 na 2002, Nyaudo alikuwa mmoja wa mabeki waliochezea Ulinzi mechi nyingi zaidi na alikuwa muhimu katika kuibua vipaji vipya wakati wa uchezaji wake.
Mwaka 2017, aliteuliwa kwa mara ya kwanza kama kocha wa muda kabla ya kuthibitishwa rasmi mwaka 2018, lakini akaondoka mwaka 2020 baada ya matokeo mabaya.
Alirejea tena Julai 2024 baada ya kipindi cha mafanikio na timu ya vijana chini ya miaka 20 (U20), ambako alisaidia kulea vipaji chipukizi.
Hata hivyo, licha ya juhudi zake za kujenga upya kikosi cha wakubwa, Ulinzi Stars walimaliza msimu wa 2024/25 katika nafasi ya 12.
