Viongozi wa chama cha ODM wamekita kambi katika eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi kwa ajili ya kumpigia debe Harrison Garama Kombe anayewania kiti cha ubunge kwenye uchaguzi mdogo ulioratibiwa kufanyika Novemba 27, 2025.
Viongozi hao waliendesha kampeni zao eneo la Garashi kisha kukamilisha na Marafa wakiwaahidi wakaazi wa Magarini kunufaika kimaendeleo iwapo watamchagua Kombe wakati wa uchaguzi huo.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ODM Gladys Wanga ambaye pia ni gavana wa kaunti ya Homabay na naibu kinara wa chama hicho Abdhulswamad Sharrif Nassir, viongozi hao walielekeza lawama kwa viongozi wa upinzani, wakisema wanaendeleza siasa za ukabila na migawanyiko.
Viongozi hao walisema chama cha ODM kinaendeleza sera za mwanzilishi wake hayati Raila Odinga za kuunganisha wakenya pamoja, wakisistiza kutoruhusu viongozi wa upinzani kupata tope chama hicho.
Hata hivyo semi za viongozi hao zilionekana kumlenga moja kwa moja kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua.
Kwa upande wake seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Madzayo, alimtaka rais William Ruto kuhakikisha anatekeleza maagizo ya ajenda 10 walizoafikiana na hayati Raila Odinga, wakati wa kutiwa saini mkataba wa serikali jumuishi, wakisema wataendelea kusalia ndani ya serikali kwa manufaa ya mwananchi.
Gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro akimpigia debe Harrison Kombe(Picha kwa hisani)
Vile vile viongozi hao waliwarai wakaazi wa Magarini kumuunga mkono mgombea wao Harrison Kombe wakati wa uchaguzi huo mdogo, wakisema hatua hiyo itamwezesha kukamilisha miradi ya maendelea aliyokuwa ameianzisha.
Taarifa ya Joseph Jira
