Msanii Sammy Kioko Aweka Gari Lake Sokoni Ili Kugharamia Matibabu ya Dada Yake

Msanii Sammy Kioko Aweka Gari Lake Sokoni Ili Kugharamia Matibabu ya Dada Yake

Mchekeshaji maarufu wa Kenya, Sammy Kioko, ametangaza kuwa ameamua kuuza gari lake ili kukusanya fedha za kugharamia matibabu ya dada yake ambaye anapitia changamoto kubwa kiafya.

Kupitia chapisho lake aliloweka kwenye Instagram Stories, Kioko alieleza jinsi uamuzi huo ulivyokuwa mgumu kwake, lakini ni hatua aliyoilazimika kuchukua kwa ajili ya familia yake.

“Asanteni kwa simu, maombi na maneno ya faraja. Kwa wanaonijua, hii gari imekuwa baraka yangu kwa miaka minane. Wale ambao wamekuwa wakinifuatilia kwa miaka kumi wanajua nilivyopata gari hili. Wakati mwingine, kama mwanaume, lazima ufanye kile kinachopaswa kufanyika hata kama kinauma,” aliandika.

Akiendelea kueleza, Kioko alisema kuwa hataki kusema kuwa “anauza gari”, bali anataka kubariki mtu nalo kwa bei nzuri.”

“Mwezi huu wa Novemba nilikuwa nimepanga kumsafirisha dada yangu kwenda kutafuta matibabu. Hata hivyo, muda si rafiki wetu,” aliongeza kwa huzuni.

Kioko, ambaye amekuwa akijulikana kwa ucheshi wake katika jukwaa la Churchill Show na kazi zake za mtandaoni, amepokea wimbi la faraja na sala kutoka kwa mashabiki na marafiki mitandaoni.

Wengi wamemsifu kwa moyo wake wa kujitolea na upendo wa kifamilia, wakimtakia dada yake afya njema na uponyaji wa haraka.

Chapisho hilo limekuja siku chache baada ya Sammy Kioko kushiriki picha kwenye ukurasa wake wa Facebook, ikimuonesha dada yake akiwa hospitalini akipokea matibabu.

Katika maelezo yaliyofuatana na picha hiyo, Kioko alionyesha kukatishwa tamaa kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya mradi ambao anadai aliukamilisha kwa Serikali ya Kaunti ya Machakos — fedha ambazo amesema ni muhimu kugharamia matibabu ya dada yake yanayoendelea.

“Ukiamua kunyamaza katika hali ya dhuluma, basi umechagua upande wa mnyanyasaji! Hakuna mtu anaomba misaada ya bure — ni malipo ya kazi iliyofanywa. Hiyo ilikuwa upasuaji wake wa kwanza. Tumekuwa tukirudi hospitalini kwa ukaguzi wa kawaida, tukingoja na kuomba tulipwe angalau kugharamia upasuaji wa pili unaotakiwa kufanyika,” aliandika.

Kioko aliendelea kuiomba serikali ya kaunti kuweka utu mbele kuliko siasa, akidai kwamba jitihada za familia yake za kuomba msaada zimegeuzwa suala la kisiasa.

“Serikali ya kaunti, tuweke utu mbele — si kila kitu kiingizwe kwenye siasa! Tuliomba msaada, lakini tukageuzwa mazungumzo ya kisiasa. Hii si haki. Tunachohitaji ni malipo yetu tu,” aliongeza kwa hisia.