Dkt Amoth: Asilimia 80 ya wakenya wanaishi na magonjwa ya Meno

Dkt Amoth: Asilimia 80 ya wakenya wanaishi na magonjwa ya Meno

Mkurugenzi wa Afya nchini Dkt Patrick Amoth amesema asilimia 80 ya wakenya wanaishi na magonjwa ya Meno kutokana na kukosa kuzingatia afya ya meno kikamilifu.

Dkt Amoth alitaja uvutaji wa sigara na utumizi wa vyakula vya sukari kupita kiasi kama sababu kuu ya magonjwa ya meno.

Akizungumza na Wanahabari baada ya kufungua rasmi Kongamano la kujadili changamoto za afya ya meno katika eneo la Diani kaunti ya Kwale, Dkt Amoth alisema mikakati ya kuhakikisha magonjwa ya Meno yanajumuishwa katika bima ya afya ya SHA imeafikiwa.

“Tumekuja hapa kutafakari mbinu gani zitasaidia kukabiliana na changamoto ambazo zipo kwani idadi kubwa ya wakenya wanakabiliana na tatizo la meno na hii imechangia sana na kutozingatia afya ya meno”, alisema Dkt Amoth.

Kwa upande wake rais wa Muungano wa madaktari wa meno nchini Dkt Kahura Mundia alisema Kenya inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madaktari wa meno, akiitaka serikali kuhakikisha inajiri madaktari wa meno wa kutosha.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi