Mwanamuziki wa muziki wa kufoka (hip-hop) Kaa la Moto ameendelea kuthibitisha kuwa bado ni nguzo muhimu katika harakati za muziki wa Pwani, baada ya kuachia wimbo wa dakika 8:45 unaojulikana kama ‘Funga File Cypher’.
Wimbo huo umeleta pamoja wasanii kadhaa wanaounda taswira halisi ya hip-hop ya Pwani, wakionyesha mitiririko, misemo na maudhui yanayogusa maisha halisi ya vijana na jamii kwa ujumla.
Katika cypher hiyo, Kaa la Moto amewashirikisha Simba Zee, Black Mtengwa, Tricks, Tylo Mil, Chibo Dee, Survivor, Musa Kiama, Young Njita, Ohms Law Montana, Emkay 64, na Reagan Dandy.
Kila msanii ameleta ladha yake ya kipekee — kuanzia mitindo ya haraka, mafumbo ya kiundani, hadi uchezaji wa maneno unaobeba utambulisho wa Pwani.
Sekunde 16 za Moto
Ingawa Kaa la Moto anaonekana kuimba kwa sekunde 16 pekee, sehemu hiyo imenifanya kuwaza kwa kina. Mistari yake fupi lakini yenye uzito mkubwa imenigusa. Baadhi ya vipande ambavyo vimeniacha nikijiuliza maswali:
- Wasanii wa playback wanatuulia bendi na gemu,
- Nimekuja kuchukua kile mulinyima Kantai,
- Nilirudisha rap baada ya madingi kuiacha,
- Nilifanya mama kuwa shabiki na mwanzoni alikuwa hapendi,
- Na kama pesa haitoshi na show siendi.
Je, Kaa la Moto anakemea wasanii wa playback, akisisitiza umuhimu wa uhalisia na uhai wa muziki? Je, anamuenzi marehemu Kantai, akionyesha kuwa anakuja kurudisha hadhi ya hip-hop iliyoachwa na wakongwe? Je, anajivunia mapinduzi yake binafsi, akionyesha safari yake kutoka kukataliwa hadi kuheshimiwa? Je anaweka kipaumbele kwa thamani kuliko tamaa, akisema wazi kuwa bila malipo halali, hafanyi onyesho?
