Mshukiwa wa mauaji kuzuiliwa rumande kwa siku 7

Mshukiwa wa mauaji kuzuiliwa rumande kwa siku 7

Mahakama ya Kilifi imeagiza kuzuiliwa rumande mshukiwa wa mauaji ya Ruth Ochieng’ mwenye umri wa miaka 60 kutoka kaunti ya Kisumu baada ya mshukiwa Evans Otieno kukamatwa katika Kanisa la Newlife Prayer Center lililoko eneo la Mavueni kaunti ya Kilifi.

Otieno alitiwa nguvuni na maafisa wa usalama alipokiri kwamba alitekeleza mauaji hayo mbele ya Mchungaji wa Kanisa hilo Ezekiel Odero, akitaka aombewe kama hatua moja wapo ya kutubu dhambi zake.

Hakimu wa Mahakama ya Kilifi Charles Obulutsa amesema Otieno atazuiliwa rumande kwa siku 7 ili kumuwezesha afisa wa polisi wa kituo cha polisi cha Seme mjini Kisumu anayechunguza kesi hiyo kufika Mahakamani.

Hakimu Obulutsa, ameeleza Mahakama kwamba wakati afisa huyo wa Polisi atakapofika katika Mahakama ya Kilifi atapewa idhini ya kumchukua mshukiwa ili afunguliwe mashtaka ya mauaji mjini Kisumu.

Awali Mahakama ilielezwa kwamba mwili wa mahehemu ulipatikana na kuthibitishwa kwamba alikuwa amenyongwa na uchunguzi zaidi ulikuwa unaendelea kabla ya mshukiwa kukamatwa katika maeneo ya Kanisa la Newlife Prayer Centre, eneo la Mavueni kaunti ya Kilifi.

Kesi hiyo itatajwa tena Februari 11 katika ili kuwakabidhi maafisa wa Polisi kutoka kaunti ya Kisumu mshtakiwa huyo.

Taarifa ya Teclar Yeri