Imebainika kuwa idadi kubwa ya wanawake na vijana katika kaunti ya Kilifi bado hawajahamasishwa vilivyo kuhusiana na masuala ya uongozi, uundaji wa bajeti na sera katika serikali za kaunti na serikali kuu.
Katika kikao cha uzinduzi wa mradi wa meaningful Engagement And Transformative Action ( META) ambacho kimeandaliwa na Shirika la Timiza Youth Initiative na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali, viongozi wa kaunti ya Kilifi, waandishi wa habari, vijana na akina mama.
Kulingana na Mwenyekiti wa Shirika la Timiza Youth Initiative Brian Mundia, hatua ya kuwatenga vijana na akina mama pamoja na wadau mbalimbali katika kutoa maoni yao kuhusu miradi ya maendeleo kumechagia wengi wao kusalia nyuma katika masuala yanayohusu maendeleo, uongozi na matumizi ya mitandao.
Mundia alisema mradi huo ambao pia unawalenga watu walio na uatilifu, wanapania kuzuru hadi maeneo ya mashinani kuhakikisha kuna hamasa ya kutosha na namna ya kutumia mitandao ya kidijitali kujibunia nafasi za ajira na wanashirikiana na wizara ya jinsia ile ya ugatuzi na mazingira kaunti ya Kilifi ili kufanikisha suala hilo.
Kwa upande wake Jackline Waweru wa shirika la Leadership For Impact, alisisitiza umuhimu wa vijana na akina mama kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kushiriki upigaji wa kura ili kuwaepusha kutumiwa visivyo na wanasiasa.
Ni kauli ambazo ziliungwa mkono na Waziri wa ugatuzi kaunti ya Kilifi, Clara Chonga ambaye alisema wanaweka mikakati kuhakikisha Wananchi wa kaunti ya Kilifi wanaweza kushiriki zoezi la ukusanyaji wa maoni pia kupitia mfumo wa kidigitali.
Taarifa ya Janet Mumbi
