Wakaazi wa Taru kaunti ya Kwale wanufaika na mradi wa maji

Wakaazi wa Taru kaunti ya Kwale wanufaika na mradi wa maji

Halmashauri ya kupambana na ukame nchini NDMA ikishirikiana na serikali ya kaunti ya kwale imewakabidhi rasmi wakaazi Taru wadi ya Macknon mradi wa maji wa Taru-Roka-Egu-Kwa Kalinga uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 24.

Akizungumza wakati wa hafla hio huko Taru, mkurugenzi mtendaji wa NDMA nchini Hared Aden alisema kuwa mradi huo utafaidi moja kwa moja wakaazi 3,347 na zaidi ya mifugo elfu 5.

Aden alidokeza kuwa hatua hio sasa imetatua tatizo sugu la ukosefu wa maji lililokuwa likiwakumba wenyeji.

Kwa upande wake mwenyekiti wa bodi ya NDMA Shallow Yahya alisema kuwa serikali ya kitaifa iko mstari wa mbele kuangazia na kutatua changamoto zinazowasibu wakaazi ili kuboresha maisha na kipato chao.

Wakaazi waliofaidika na mradi huo walipongeza hatua ya serikali kuwaletea bidhaa hio karibu huku gavana wa Kwale Fatuma Achani akipongeza NDMA kwa kushirikiana na serikali ya kaunti katika masuala ya kuwasaidia wakaazi na huduma msingi.

Taarifa ya Mwanahabari wetu