Wamiliki hoteli zilizofungwa kaunti ya Kilifi wameshinikizwa kuhakikisha wanaziuza kwa wawekezaji wengine iwapo wameshindwa kurejesha huduma katika hoteli hizo.
Akizungumza na vyombo vya habari gavana wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika ikizingatiwa kwamba ni mojawapo ya kitega uchumi cha kaunti hii ya Kilifi.
Aidha gavana Mung’aro ameeleza matumaini ya kuimarika kwa sekta hiyo baada ya kupatikana kwa masoko kwenye mataifa mbalimbali ya ulaya.
Kwa upande wake waziri wa utalii na biashara kaunti ya Kilifi Raymond Ngala amehoji kuwa serikali ya kaunti itajizatiti kuboresha sekta hiyo hasa kupitia wa michezo.
Ngala amesema kuwa sekta ya utalii iko na uwezo wa kubuni nafasi nyingi za ajira kwa vijana na kupunguza changamoto ya ukosefu ajira, hivyo serikali itahakikisha kuwa sekta hiyo inaboreshwa.
“Wale wenye hoteli ambao wanashindwa kuendeleza biashara hiyo wapeane hoteli hizo kwa wawekezaji wengine ili kuendeleza shughuli badala ya kuziacha bila kuendelea ikizingatiwa kuwa uchumi wa kaunti hii unategemea hoteli hizo kupokea wageni.” alisema Ngala.
Taarifa ya Pauline Mwango.
