Ikiwa imeungwa mkono na umati mkubwa wa mashabiki waliofurika Kasarani Indoor Arena, Nairobi City Thunder iliibwaga Johannesburg Giants ya Afrika Kusini kwa ushindi wa 94–84, na kutwaa taji la Road to BAL East Division katika fainali yenye msisimko mkubwa usiku wa Jumapili.
Ushindi huo uliihakikishia Thunder ubingwa wa pili mfululizo wa East Division Elite 16, mafanikio ya kihistoria yaliyosherehekewa na mashabiki zaidi ya 5,000 walioujaza ukumbi hadi kufikia kiwango cha juu kabisa.
Thunder na Giants zote zilikuwa tayari zimefuzu kwa Basketball Africa League (BAL) ya mwaka 2026 baada ya kufika fainali, lakini ilikuwa ni miamba wa Kenya — waliokuwa wenyeji wa mashindano kwa mwaka wa pili mfululizo — waliothibitisha ubabe wao kwenye ardhi ya nyumbani.
Thunder yapaa tangu nusu fainali
Chini ya kocha Brad Ibs, Thunder ilikuwa tayari imetia kibindoni tiketi ya BAL baada ya ushindi wa kishindo wa 109–70 dhidi ya Ferroviario de Beira ya Msumbiji katika nusu fainali.
Wakipanda juu ya kasi hiyo, waliutawala mchezo wa fainali mapema, wakichukua robo ya kwanza kwa 28–17, na kuongoza ya pili 22–21 na hivyo kwenda mapumzikoni wakiwa mbele 50–38.
Thunder waliendeleza moto wao kipindi cha tatu, wakiwazidi Giants 33–23. Hata hivyo, Afrika Kusini walijaribu kurejea mchezoni na kushinda robo ya nne 23–11, lakini uongozi wa mapema wa Thunder uliwahakikishia ushindi wa 94–84.
Ongwae na Majok waangaza, Adera aperform kivyake
Nahodha Tylor Ongwae na mchezaji wa kati Ater Majok waliiongoza Thunder kwa alama 17 kila mmoja na rebounds nne, huku Albert Odero akiongeza alama 14.
Lakini ilikuwa ni Eugene Adera aliyeng’ara kwa mchango muhimu, akivuna rebounds 12 na assists 8, akicheza jukumu muhimu sana katika ushindi wa timu katika pande zote mbili za uwanja.
