Mkufunzi wa Nigeria Eric Chelle ameishutumu DR.Congo kufanya uchawi katika mechi ya kufuzu kombe la dunia dhidi ya Nigeria

Mkufunzi wa Nigeria Eric Chelle ameishutumu DR.Congo kufanya uchawi katika mechi ya kufuzu kombe la dunia dhidi ya Nigeria

Kocha wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Nigeria ameituhumu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo) kwa kufanya “uchawi” baada ya ndoto za kikosi chake kufuzu Kombe la Dunia 2026 kukatishwa kwenye mikwaju ya penalti.

DR Congo na Nigeria zilitoka sare ya 1-1 baada ya muda wa nyongeza katika fainali ya mchujo wa Afrika mjini Rabat Jumapili, na timu ya Afrika ya Kati ikashinda 4-3 kupitia penalti na hivyo kujipatia nafasi ya kucheza mchujo wa mabara utakaofanyika Mexico Machi mwakani.

Katika mahojiano yake na wanahabari baada ya mechi, kocha Eric Chelle alisema mwanachama mmoja wa timu ya DR Congo “alikuwa akifanya uchawi, kila wakati, kila wakati, kila wakati”.

“Hiyo ndiyo sababu nilikuwa na wasiwasi kidogo,” alisema Chelle, aliyewahi kuwa mchezaji wa Mali, ambaye tangu achukue usukani wa Super Eagles amepata ushindi minne na sare mbili kwenye mechi za mashindano.

Chelle alikuwa amekiri kabla ya mechi kuwa ingekuwa “ngumu sana Morocco”.

Akitumia ishara za mikono, alisema alimwona mmoja wa benchi la DR Congo akipeperusha mkono kana kwamba ananyunyiza kitu. “Sijui kama ni maji au kitu kingine kama hicho.”

Katika mchakato wa matuta uliokuwa na wasiwasi mkubwa, ambapo penalti nne ziliokolewa na nyingine moja ikakosa kabisa, nahodha wa DR Congo Chancel Mbemba alipuuzilia mbali chupa iliyotupwa kuelekea kwake na mvua kubwa, na akapiga penalti ya ushindi. DR Congo sasa wanatafuta kurejea kwenye mashindano ya Kombe la Dunia baada ya kukosekana kwa muda mrefu.

Nigeria, ambao ni moja ya nguvu kubwa za soka barani Afrika, wako nafasi 19 juu ya DR Congo katika viwango vya dunia na walikuwa wanaopewa nafasi kubwa kabla ya mechi.