Murkomen ahimiza ushirikiano wa pamoja na wadau wa masuala ya ubaharia

Murkomen ahimiza ushirikiano wa pamoja na wadau wa masuala ya ubaharia

Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen, ametoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya washirika na wadau ili kuimarisha usalama wa baharini na maziwa makuu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamano la kamati ya uongozi wa Jukwaa la ushirikiano wa taarifa ya kanda ya Indo-Pasifiki (IORIS) lililofanyika mjini Mombasa, Waziri huyo alisisitiza kuwa ushirikiano wa mapema ni muhimu katika kukabiliana na vitisho vinavyoibuka vya usalama wa baharini.

“Ushirikiano wa mapema na muhimu katika kulinda usalama wetu wa baharini,” alisema Murkomen.

Kongamano hilo la siku tatu linaandaliwa kwa pamoja na huduma ya Walinzi wa Pwani ya Kenya (KCGS) pamoja na mradi wa njia muhimu za baharini wa Indo-Pasifiki unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU-CRIMARIO), ukiwaleta pamoja wadau wa usalama wa baharini..

Mradi wa EU-CRIMARIO umeundwa kuimarisha usalama na ulinzi wa baharini kupitia kuboreshwa kwa ushirikiano wa taarifa na uratibu wa operesheni.

Kongamano la siku tatu la kamati ya uongozi la Jukwaa la ushirikiano wa taarifa ya kanda ya Indo-Pasifiki (IORIS), Mombasa

Mpango wake mkuu, IORIS, ni jukwaa salama na lisiloegemea upande wowote linalotumia mtandao, unaounganisha zaidi ya mashirika 150 kutoka nchi 70, na kuwezesha uratibu wa operesheni za baharini kwa wakati halisi.

Kauli za Murkomen ilijiri kufuatia tangazo la Rais William Ruto kwamba kampuni ya usafiri wa baharini ya Norway, Wilhelmsen, itaajiri mabaharia 1,000 kutoka Kenya, baada ya mazungumzo na kampuni hiyo.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi wa EU-CRIMARIO Martin Cauchi Inglott, Mkurugenzi mkuu wa huduma ya walinzi wa Pwani ya Kenya Bruno Shioso, Naibu mkuu wa ujumbe wa umoja wa Ulaya nchini Kenya Ondrej Simek, pamoja na washkadau wengine.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi